Tunamfahamu kama bwana afya, na hii ni kutokana na uwezo aliojaliwa
Muumba wa kuweza kula mpaka mifupa. Wengi wetu hatufahamu gharama
anayoipata fisi kutokana na kuwa na uwezo huo wa kula mifupa, kwato
mpaka pembe za wanyama wengine. Ni kwamba, Mfumo wa mmeng'enyo wa fisi
una tindikali ambazo ndizo zinampa kiburi mnyama huyu kupambana na
mifupa iliyowashinda wenzie. tindikali hizi hufanya kazi ya kumeng'enya
bidhaa zote ambazo Fisi huzitupiamo kinywani mwake. Zoezi la kumeng'enya
mifupa na vyakula vingine huishia kuzalisha joto kali sana kwenye mwili
wa fisi. Endapo fisi hatachukua hatua stahiki joto lile linaweza
kupanda na kufikia viwango vya hatari vyenye kuweza kuhatarisha maisha
yake. Joto huwa kali kiasi cha kuweza kuanza kuharibu baadhi ya viungo
vyake vya ndani.
ili kuweza kukabiliana na joto hilo na pia kunusuru maisha yake, fisi
hulazimika aidha kutafuta mahali ambapo kuna kivuli au Sehemu yenye maji
au Tope. Sehemu hizi ndizo ambazo Fisi atazitumia kujaribu kupunguza
makali ya joto ili lisimletee madhara zaidi. Chaguo la namna ya
kujihifadhi hutegemea na mazingira aliyopo. Mathalani kwa fisi hawa
tuliowakuta ndani ya Hifadhi ya Serengeti walilazimika kujitosa kwenye
matope yaliyokuwa kandokando ya barabara ya Serengeti- Ngorongoro. hii
ni kwasabu eneo ambalo tuliwakuta fisi hawa, hakukuwa na kichaka au mti
wa kuweza kuwapa kivuli kizuri kupumzika. Hali hii hupelekea pia fisi
kupenda kufanya mawindo yake usiku ambako hali ya joto huwa ni ya chini.
Jua la mchana na shibe ni mateso kwa bwana afya.
No comments:
Post a Comment