nmb

nmb

Saturday, August 4, 2012

Cheki Utajiri wa wabunge unavyotisha




SAKATA la wabunge saba kuhusishwa kuomba na kupokea ‘kitu kidogo’ lililotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu limeingia katika sura mpya baada ya wananchi kuhamaki kwa habari zilizoripotiwa wiki hii kuwa kuna wabunge wana utajiri wa kupitiliza, Risasi Jumamosi linashuka nayo.
Baadhi ya wapiga kura wamesema kuwa kama ni kweli kuwa waheshimiwa hao wana utajiri mkubwa kiasi hicho, itabidi kuwafikiria upya mwaka 2015 kwa kuwa hakuna sababu ya kumpa kura mtu ili akale huku wapiga kura wakishinda na njaa.
Yapo madai mazito kwamba baadhi ya wabunge hao wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika wa Bunge, Anna Makinda wanamiliki maghorofa, magari ya kifahari wanayokodisha, vituo vya mafuta huku wengine wakidaiwa kuwa wazabuni wa mafuta migodini na wamiliki wa makampuni ya utalii (tours).
Wabunge wa CCM waliotajwa na Lissu kuhusishwa na kashfa hiyo na majimbo yao kwenye mabano ni Nassir Abdallah (Korogwe Mjini), Mariam Kisangi (Viti Maalumu), Vicky Kamata (Viti Maalumu) na Charles Mwijage (Muleba Kaskazini) ambao hata hivyo, wote wamekanusha madai hayo.
Wabunge wengine watatu waliotajwa na Lissu tumeshindwa kuwataja kwa kuwa hawakupatikana kuzungumzia tuhuma dhidi yao.
Katika orodha hiyo wamo wawili wa viti maalumu na mmoja wa jimbo ambapo Lissu alidai kwamba wamekuwa wakishiriki vikao vya Kamati ya Nishati na Madini huku wakijua kuwa wana maslahi binafsi na wengine kutumia fursa hiyo kujinufaisha na kuwaacha wapiga kura wao katika maisha magumu.
Hata hivyo, Lissu alisema wabunge wa Chadema ambao walikuwa katika Kamati ya Nishati na Madini, John Mnyika, David Silinde na Mwanamrisho Abama hawahusiki na mlungula na kama kuna mtu ana ushahidi dhidi yao apelekewe.
Lissu alisema wabunge  wawili (majina tunayahifadhi), wamejihusisha kufanya biashara na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) hivyo wana mgongano wa kimaslahi.
Alisema Mwijage ana mgongano wa kimaslahi katika mchakato wa kuipa zabuni ya kusambaza mafuta Kampuni ya Puma Energy kwa kuwa yeye ni mtalaamu mzuri wa kampuni hiyo ambayo serikali inamiliki hisa kwa asilimia hamsini.
“Nassir Abdallah na Mariam Kisangi wanadaiwa kumiliki vituo vya mafuta. Sasa kwa namna yoyote ile kuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini hawawezi kutendea haki mchakato wowote unaohusu mafuta,” alisema Lissu.

MANENO YA MBUNGE KISANGI
Hata hivyo, Kisangi alipoulizwa kuhusu kumiliki kituo cha mafuta alikiri lakini akasema ni biashara ya ndugu zake huku akijitetea kwamba sheria haimzuii.
MBUNGE MWIJAGE NAYE
Kwa upande wake, Mwijage alikanusha kuhusika na kuielekeza chochote  Kampuni ya Puma.
“Si kweli. Mimi ni mtaalamu wa petroli ambaye kimsingi nina faida kubwa bungeni na kwenye jamii kwa jumla. Sijafanya maamuzi yoyote ya kulihujumu taifa,” alisema.
NASSIR PIA HAKUBAKI NYUMA
Mbunge Nassir ambaye ni wa CCM, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na madai hayo, alikanusha kumiliki vituo vya mafuta.

ZITO KABWE NDANI YA MJADALA
Zitto Kabwe ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa ‘leseni’ ya Chadema lakini  pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba ni kweli alihojiwa na sekretarieti ya chama chake kutokana na tuhuma za rushwa zinazowagusa baadhi ya waheshimiwa.
“Nilijieleza kwa saa tatu mbele ya sekretarieti ya chama kuhusu tuhuma za rushwa dhidi yangu. Niliomba kutoa maelezo kwa katibu mkuu, nimekiomba chama kufanya uchunguzi na ikibainika ni kweli hatua zichukuliwe dhidi yangu.”
Aidha, Lissu alimtaja mbunge mmoja (jina limehifadhiwa) kuwa alikuwa  akiyafanyia kampeni ya kupata zabuni makampuni ya mafuta ya Oryx na Camel, akadai mheshimiwa huyo wa kike ana uhusiano wa kimapenzi na kigogo mmoja katika Wizara ya Nishati na Madini Tanzania.

OLE SENDEKA AWAKA
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka ameonesha kiu ya kumburuza kortini Lissu akidai amemchafua. Wabunge wengine waliotajwa katika kashfa hiyo hawakuweza kupatikana kuzungumzia tuhuma hizo zilizotolewa na Lissu.

TAKUKURU Kutokana na madai hayo mazito, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai alisema kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilikuwa ikiendelea kuwahoji baadhi ya wabunge kuhusu tuhuma zinazowakabili na kwamba uchunguzi ukikamilika taarifa zitawekwa hadharani. Kamati ya Nishati na Madini ilikuwa ikiundwa na Selemani Zedi (Mwenyekiti), Diana Chilolo (Makamu M/kiti), Haji Khamis, Catherine Magige, Abia Nyabakari, Dr. Festus Limbu, Eng. Athuman Mfutakamba na Lucy Mayenga. Wengine ni Josephine Changula, Mwanamrisho Taratibu, Suleiman Nchambi, Ally Mbarouk Salim na  Kisyeri Chambiri.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

AddThis