Hapo mwanzo, yasemekana kuwa Kinyonga alikuwa na mwendo wa haraka na
hata kukimbia kwa kasi kama wanyama wengine. Hakuwa na mwendo wa
kusuasua kama tumwonavyo siku hizi. Je, ni kitu gani kilichomfanya
Kinyonga awe hivi alivyo?
Siku moja, lilipogwa la mgambo la kuwataka wanyama wote wakusanyike pamoja ili kuwe na mashindano ya kukimbia, wapate kujua ni mnyama gani hodari wa kuchanganya miguu kushinda wengine. Taratibu zilifanyika ili kuweka mambo yote sawa. Siku ya siku ilipowadia, mashindano ya kukimbia yakaanza:
Msimamizi wa mashindano alianza kuhesabu: Moja, mbili, tatu!
Loo, vumbi likaanza kutimka kutokana na kishindo cha mbio za wanyama
wale. Kwa vile mbio zilikuwa za kasi sana, baadhi ya wanyama walioweka
vitu mfukono mwao, vikaanza kudondoka, kimoja baada ya kingine. Kinyonga
kutokana na ukali wa macho yake, akaviona vitu hivyo. Kadiri mbio
zilivyozidi kupamba moto, na ndivyo vitu viliendelea kudondoka.
Hatimaye, Kinyonga akashindwa kujizuia. Vitu vile vilimtinga sana.
Akabadili uelekeo.
Akawapisha wanyama wengine na kujifanya kama vile
anakwenda kujisaidia. Kumbe, anarudi nyumba na kuanza kuokota vitu
vilivyodondoshwa na wanyama wenzake. Kwa kuwa vitu vile vilikuwa vingi
na vilidondoka ovyo ovyo bila mapangilio wowote, Kinyonga alianza kwenda
polepole, kwa maringo na makini, ili aweze kuokota vizuri vitu vyote
kisiachwe hata kitu kimoja. Alifanya hivyo sio kwa ajili ya kuwarejeshea
wale waliopoteza, la hasha, bali kuweka kibindoni, ili vimfae mwenyewe
maishani.
"Tamaa mbele, mauti nyuma." Sasa basi, kutokana na tamaa hiyo, alikiona cha mtema kuni. Jamaa tangu siku ile, hadi leo hii, hakuweza tena kutembea haraka wala kukimbia. Akawa "amejitaiti" mwenyewe. Halafu, akawa anabadilika badilika rangi kufuatana na mazingira ya sehemu anayokuwepo ili asije akaonwa na wenye mali zao. Vile vile, anazungusha zungusha macho huku na huko kana alivyofanya siku ili "alipookota" vitu vilinyodondoshwa na wanyama wenzake.
Na Kat.V.A. Ndunguru kutoka gazeti la Mlezi.
Je hadithi hii wewe msomaji inakufundisha nini?
No comments:
Post a Comment