Wizara
ya Maliasili na Utalii itaendesha zoezi la kuwaangamiza kunguru weusi
katika mikoa ya Tanga na Pwani kuanzia tarehe 2 Oktoba hadi 1 Novemba
2012 kwa kutumia sumu tulivu aina ya DRC 1339. Zoezi hilo limehamia
katika mikoa hiyo baada ya kukamilika mkoani Dar es Salaam ambako
liliendeshwa kwa mwezi mzima tangu tarehe 27 Agosti 2012 hadi 25
Septemba 2012.
Katika zoezi hilo jumla ya kunguru 41,487 waliuwawa Jijini Dar es
Salaam.
Aidha, tangu Mradi wa kudhibiti kunguru weusi uanze Mwezi Julai
2010, hadi Septemba 2012 jumla ya kunguru weusi 807,961 wameshauawa kwa
kutumia sumu hiyo ya DRC 1339 na mitego katika Mikoa ya Dar es salaam,
Morogoro, Pwani na Tanga. Ingawaje sumu hiyo haina madhara makubwa kwa
binadamu, wananchi hasa watoto, wanatakiwa kutochezea mizoga ya kunguru
ambao watakuwa wamekufa kutokana na sumu hiyo.
Endapo mtu atakuwa ameishika mizoga hiyo anatakiwa anawe kwa sabuni.
Kunguru weusi wanauwawa kwa lengo la kupunguza idadi yao ili wasiendelee
kusababisha kero kwa wananchi kwa kupokonya chakula na vitu mbalimbali.
Aidha, kunguru wamekuwa wakieneza vimelea vya magonjwa mbalimbali kwa
binadamu na kuku. Wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa vikosi
ambavyo vitakuwa vinaokota mizoga ya kunguru, kwa kuonyesha iliko.
Pia wanatakiwa kutoa taarifa pale watapogundua kuwa kuna idadi kubwa ya
ndege hao sehemu yoyote ili hatua za kuwaangamiza ziweze kuchukuliwa.
Taarifa zipelekwe katika ofisi za Maliasili za Mikoa, Wilaya, na
Manispaa. Pia wanaweza kupiga simu 0716 129120 kwa Mkoa wa Pwani na 0757
585358 kwa Mkoa wa Tanga.
Zoezi la kuwaangamiza kunguru weusi
litahamia mkoani Morogoro tangu tarehe 5 Novemba 2012 ambako
litaendeshwa kwa muda wa mwezi mzima.
Baada ya kumalizika kwa zoezi katika mkoa huo Wizara itafanya tathmini
ili kuona mafanikio ya operesheni hii. Tathmini katika mikoa yote minne
(Dar es Salaam, Pwani, Tanga, na Morogoro) itafanyika kwa pamoja kwa
kuwa kunguru wanaoonekana katika mkoa mmoja ndiyo walewale ambao
huzungukia mikoa yote inayopakana nao.
George Matiko, MSEMAJI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII 1 Oktoba 2012
Simu :
+255 784 468047
No comments:
Post a Comment