nmb

nmb

Wednesday, November 28, 2012

Michoro Ya Kampasi Ya Muhimbili Itakayojengwa Mloganzila Kisarawe

Michoro
ya ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila iliyo kijijini Kwembe katikati ya
Wilaya za Kisarawe Mkoa wa Pwani na Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam. Hii
ni sehemu ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)
inayojengwa kwenye eneo la ekari 3800 kwa ajili ya kutolea mafunzo kwa
wanafunzi wa udaktari na huduma za Afya wapatao 15,000 kwa mwaka, na pia
itakua sehemu ya kutolea matibabu ya maradhi yote makuu na ya kawaida
nchini. Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili, ujenzi wa Hospitali hii, ambayo pesa ya ujenzi wake
imeshapatikana, unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Januari, 2013 na
unatarajiwa kukamilika miaka miwili baada ya ujenzi kuanza. Kwa maneno
mengine Kampasi ya Muhimbili ya Mloganzila inategemewa kuanza kazi
mwanzoni mwa mwaka 2015. Tayari wataalamu na wafanyakazi wanaotarajiwa
kufanya kazi katika kampasi ya Mloganzila wameshaanza mafunzo ndani na
nje ya nchi. Mara hospitali hiyo kubwa na ya kisasa itakapokamilika
itakua na uwezo wa vitanda vya kulaza wagonjwa mia sita (600). Sambamba
na kampasi ya MUHAS ya Mloganzila pia ujenzi wa Kampasi ya Afya ya Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM) umeshaanza na kufikia hatua ya juu na ambapo pia
hospitali hiyo inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2015. Kwa
mujibu wa Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (National Health
Insurance Fund) NHIF Bw. Emmanuel Humba mchakato wa kufanikisha
uanzishaji wa Chuo Hospitali hiyo vimeshaanza ambapo baadhi ya wataalamu
wakiwemo Madaktari na watumishi wengine wako nchini na nje ya nchi kwa
ajili ya masomo na mafunzo mbalimbali. Chuo hicho kinatarajia kuwa na
vifaa vya kisasa vya tiba vinavyokidhi mahitaji ya Afya na Elimu ya
Udaktari wa kiwango cha Kimataifa, ikiwa ni mikakati kabambe ya serikali
ya awamu ya nne katika kuhakikisha nchi ina wataalamu wengi na huduma
za kisasa za afya ili kuondokana na adha ya kupeleka wagonjwa nje ya
nchi kwa ajili ya matibabu. Kwa sasa MUHAS inachukua takriban wanafunzi
2442 wa udaktari na huduma za afya kwa mwaka. Hivyo ujio wa kampasi ya
Afya Mloganzila na Kampasi ya afya ya UDOM utaharakisha mpango wa
serikali wa kupunguza wastani wa wagonjwa kwa daktari mmoja kwa kiwango
kikubwa. Hivi sasa wastani ni daktari mmoja anahudumia wagonjwa 30,000.
Na Michuzi

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

AddThis