Marwa
Tawfik (Kulia) mmoja wa wajumbe waliowakilisha vyombo vya habari nchini
Misri kuja Tanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii akifafanua
jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na waandishi wa
habari (hawapo pichani) juu ya kile walichojionea walipofanya ziara
katika vivutio mbalimbali vya utalii Tanzania Bara na Zanzibar.Wengine
ni baadhi ya wawakilishi kutoka Misri.
……………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu
VYOMBO vya habari nchini Misri
vimeahidi kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini
katika kuhakikisha Tanzania inapata watalii wengi zaidi jambo
litakaloendelea kudumisha mahusiano mema yaliyopo kati ya nchi hizo.
Hayo yalisema Dar es Salaam juzi
na mmoja wa wawakilishi wa vyombo vya habari nchini Misri, Marwa Tawfik
alipozungumzia ziara waliyofanya katika vivutio vya utalii nchini ambapo
waliahidi kutumia vyombo vyao kutangaza walivyoviona.
Ujumbe wa watu sita uliowakilisha
vyombo mbalimbali vya habari nchini Misri yakiwemo magazeti na
televisheni chini ya Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo Jestas
Nyamanga walifanya ziara ya siku tano nchini kutembelea vivutio
mbalimbali vya utalii Tanzania Bara na Visiwani chini ya uratibu wa Bodi
ya Utalii nchini (TTB).
Alisema wanaporudi nchini kwao
watakaa na uongozi wa vyombo vyao na kuangalia jinsi ya kupata vipindi
maalumu katika televisheni na makala katika magazeti jambo
litakalowezesha taarifa za utalii za Tanzania kuwafikia watu wengi zaidi
nchini mwao na nchi nyingine za ukanda huo.
Tawfik alisema ana imani ziara
hiyo pamoja na kazi watakayoifanya ya kuvitangaza vivutio husika
itasaidia Tanzania kupata watalii wengi zaidi kutoka nchini mwao na
katika nchi za ukanda wa kiarabu.
“Tumeona utajiri wa asili wa ajabu
uliopo Tanzania,sisi tunaahidi kutumia vyombo vyetu kutangaza vivutio
hivi katika kuhakikisha watu wengi zaidi wanahamasika kuja Tanzania na
hatimaye kuwaongezea pato lenu kupitia utalii,” alisema Tawfik.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa TTB Aloyce Nzuki alisema ziara hiyo pamoja na nyingine ni
muendelezo wa jitihada za bodi hiyo ya kuhakikisha sekta ya utalii
inakua ndani na nje ya nchi.
Alisema ujio wa ujumbe huo kutoka
Misri utaongeza idadi ya watalii kutoka nchi hiyo pamoja na nyingize za
ukanda huo ambapo takwimu za sasa zinaonyesha Tanzania inapata watalii
25,000 kutoka nchi za ukanda huo.
Nzuki alisema pamoja na ujumbe huo
kuahidi kutumia vyombo vyao kutangaza walivyoviona pia bodi hiyo
inaendelea na jitihada za kuhakikisha matangazo ya vivutio vilivyopo
nchini yanawekwa katika lugha ya Kiswahili katika kukuza utalii wa
ndani.
“Tumekuwa na jitihada endelevu za
kuhakikisha vivutio tulivyonavyo vinajulikana ulimwenguni kote jambo
litakalosaidia kupata watalii wengi zaidi kutoka nje lakini pia
tunaendelea na jitihada za kuhakikisha utalii wa ndani unakua,” alisema
Nzuki.
No comments:
Post a Comment