nmb

nmb

Saturday, December 1, 2012

Wananchi wavamia hifadhi Serengeti wang’oa mipaka



ZAIDI ya wakazi 2,000 wa Kijiji cha Ololosokwan, wilayani Ngorongoro wakiwa na silaha za jadi, wamevamia eneo la mpaka kati yao na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuondoa nguzo za mipaka kwa madai ya hifadhi hiyo kuingilia eneo la kijiji.
Wakazi hao wakiwa na viongozi wao, Diwani wa kata hiyo, Yannick Ndoinyo na Mwenyekiti wa kijiji, Yohane ole Sainiu, walieleza wameamua kuvamia eneo hilo kuondoa nguzo zote na kuzirejesha ndani ya hifadhi baada ya kubaini mpango wa kuporwa ardhi yao.

Ndoinyo alisema wamekuwa na mgogoro wa mipaka hasa baada ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), kutaka kuweka mipaka mipya kilomita tano ndani ya kijiji chao.

“Leo wananchi wameamua wenyewe kufika hapa na kuondoa hizi nguzo ambazo zinataka kuwekwa na Tanapa katika ardhi yetu,” alisema Ndoinyo. Diwani huyo alionyesha gazeti la Serikali linalobainisha mipaka baina ya kijiji hicho na Hifadhi ya Serengeti,  toleo namba 235 la june 21 mwaka 1968 ambalo limesainiwa na hayati Julius Kambarage Nyerere.

Naye Mwenyekiti wa kijiji, Sainiu ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 30 sasa, alisema kijiji chao kwa miaka yote hakina mgogoro na Serengeti, lakini kuanzia mwaka 2008 ndipo chokochoko hizo zilipoanza.

“Tuna uhusiano mzuri kwa muda mrefu, lakini sasa limekuja hili la mipaka ndiyo sababu wananchi wamegoma kuporwa ardhi yao,” alisema Sainiu.
Naye  Mratibu wa Shirika lisilo la Serikali la Ujamaa Community Resource Team (UCRT), Konday Mako alisema wanashangaa kuibuka mgogoro huo, kwani tayari kijiji kina hati miliki baada ya kupimwa.

Mako alisema shirika lao ndilo lililohusika kupima kijiji hicho na kusaidia kupatikana kwa hati na kwamba, mipaka yote ipo wazi ila hivi sasa Serengeti kutaka kuongeza mipaka ni tatizo.
“Hapa kuna mgogoro wa mipaka, lakini mgogoro huu sasa ni wa Mkoa wa Arusha na Mara, hivyo unapaswa kutatulia kwa umakini,” alisema Mako.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, Mtango Mtahiko alikiri kuwapo kwa mgogoro huo na kwamba, hivi sasa Tanapa haina mpango wa kuweka  alama za mipaka, kwani mgogoro upo kwa waziri mkuu.“Ni kweli kuna mgogoro, lakini tulikuwa hatujafikia suala la kuweka mipaka,” alisema Mtahiko. Naye Meneja Uhusiano wa Tanapa, Pascal Shelutete alisema  wanatambua mgogoro huo lakini kuna kikao cha mwafaka kitafanyika Ijumaa hii.“Tunaomba wananchi watulie, kwani Tanapa tumepata taarifa kutakuwa na kikao Ijumaa ili kueleza juu ya hatua zilizofikiwa kuhusu mgogoro huu,” alisema Shelutete.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

AddThis