nmb

nmb

Wednesday, February 20, 2013

Sababu za kinyonga kuwa na mwendo wa kusuasua kama tumwonavyo siku hizi

Hapo mwanzo, yasemekana kuwa Kinyonga alikuwa na mwendo wa haraka na hata kukimbia kwa kasi kama wanyama wengine. Hakuwa na mwendo wa kusuasua kama tumwonavyo siku hizi. Je, ni kitu gani kilichomfanya Kinyonga awe hivi alivyo?

Siku moja, lilipogwa la mgambo la kuwataka wanyama wote wakusanyike pamoja ili kuwe na mashindano ya kukimbia, wapate kujua ni mnyama gani hodari wa kuchanganya miguu kushinda wengine. Taratibu zilifanyika ili kuweka mambo yote sawa. Siku ya siku ilipowadia, mashindano ya kukimbia yakaanza: 

Msimamizi wa mashindano alianza kuhesabu: Moja, mbili, tatu! Loo, vumbi likaanza kutimka kutokana na kishindo cha mbio za wanyama wale. Kwa vile mbio zilikuwa za kasi sana, baadhi ya wanyama walioweka vitu mfukono mwao, vikaanza kudondoka, kimoja baada ya kingine. Kinyonga kutokana na ukali wa macho yake, akaviona vitu hivyo. Kadiri mbio zilivyozidi kupamba moto, na ndivyo vitu viliendelea kudondoka. Hatimaye, Kinyonga akashindwa kujizuia. Vitu vile vilimtinga sana. Akabadili uelekeo. 

Akawapisha wanyama wengine na kujifanya kama vile anakwenda kujisaidia. Kumbe, anarudi nyumba na kuanza kuokota vitu vilivyodondoshwa na wanyama wenzake. Kwa kuwa vitu vile vilikuwa vingi na vilidondoka ovyo ovyo bila mapangilio wowote, Kinyonga alianza kwenda polepole, kwa maringo na makini, ili aweze kuokota vizuri vitu vyote kisiachwe hata kitu kimoja. Alifanya hivyo sio kwa ajili ya kuwarejeshea wale waliopoteza, la hasha, bali kuweka kibindoni, ili vimfae mwenyewe maishani.

"Tamaa mbele, mauti nyuma." Sasa basi, kutokana na tamaa hiyo, alikiona cha mtema kuni. Jamaa tangu siku ile, hadi leo hii, hakuweza tena kutembea haraka wala kukimbia. Akawa "amejitaiti" mwenyewe. Halafu, akawa anabadilika badilika rangi kufuatana na mazingira ya sehemu anayokuwepo ili asije akaonwa na wenye mali zao. Vile vile, anazungusha zungusha macho huku na huko kana alivyofanya siku ili "alipookota" vitu vilinyodondoshwa na wanyama wenzake.

Na Kat.V.A. Ndunguru kutoka gazeti la Mlezi.
Je hadithi hii wewe msomaji inakufundisha nini?

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

AddThis