Na Sophia Fundi, Karatu
MBUNGE wa Karatu, mkoani Arusha, Mchungaji Israel Natse, ameutaka uongozi wa Wilaya hiyo kulipatia ufumbuzi tatizo la uharibifu wa chanzo cha maji cha Qangded.
Chanzo hicho kipo katika Kata ya Mangola, wilayanikaratu ambapo Mchungaji Natse, aliwataka viongozi husika kuacha siasa kabla wananchi hawajachukua sheria mkononi.
Mchungaji Natse aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Jobaj, Kata ya Mangola na kuwataka wananchi kuwacharaza viboko watendaji wa vijiji ambao watashindwa kutekeleza majukumu waliyonayo katika jamii.
Alisema kitendo cha uongozi wa Wilaya hiyo kushindwa kutatua mgogoro huo ambao umedumu muda mrefu kati ya watu wenye uroho wa mali na kuanzisha kimewashangaza wananchi.
“Haiwezekani Serikali ishindwe na watu wachache na kuwawekea mipaka wananchi ndani ya nchi yao, hivi karibuni Mkuu wa Wilaya hii aliwaweka chini ya ulinzi waharibifu wa chanzo cha maji na kuwaamuru wasimamishe shughuli zote ndani ya chanzo hiki.
“Jambo la kushangaza, baada ya watu hawa kuachiwa waliendelea na uharibifu na kuwatambia wananchi hivyo ni wazi wanatetewa na viongozi wa CCM kwa kivuli cha ukada wa chama chao,” alisema.
Aliongeza kuwa, jambo hilo ni hatari kwa maisha ya wananchi wa kata hiyo kwani tegemeo lao ni chanzo hicho kwa kwa ajili ya kilimo cha vitunguu, mpunga na mahindi.
“Haya yote yanatokana na Serikali legelege, katika kata hii kila mtu akiamka asubuhi anaweza kujiamulia kwenda kufyeka chanzo hiki bila kiongozi yeyote kumuuliza,” alisema.
Mchungaji Natse aliongeza kuwa, hivi sasa katika chanzo hicho kuna pampu za maji zaidi ya 30 ambazo zimewekwa na watu mbalimbali lakini Serikali bado imekaa kimya.
“Kila mtu mwenye pampu katika chanzo hiki ahakikishe anaitoa, haijalishi yupo chama gani cha siasa kabla wananchi hawajachukua sheria mkononi,” alisema Mchungaji Natse.
Chanzo: Gazeti Majira
No comments:
Post a Comment