Taarifa hii inatoa mrejeo wa hali ya joto la bahari (El Niño na La Niña) kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, 2012.
Hali ya sasa na mwelekeo wa Hali ya joto la Bahari:
Katika
kipindi cha Julai hadi Septemba, 2012, hali ya joto la bahari ukanda wa
tropikali wa Bahari ya Pasifiki iliongezeka na kuwa juu ya wastani hali
iliyoashiria kuwepo kwa El Niño hafifu, hata hivyo hali ya mifumo ya
upepo, mgandamizo wa hewa katika usawa wa bahari na mawingu vilishindwa
kuwiana na ongezeko hilo hafifu la joto la bahari.
Katika
kipindi cha miezi ya hivi karibuni hadi sasa hali ya joto la bahari
katika ukanda wa tropikali wa Bahari ya Pasifiki imekuwa ya wastani,
hali hii haiashirii kuwepo kwa aidha El Niño au La Niña. Aidha katika
ukanda wa Bahari ya Hindi unaopakana na nchi yetu pamoja na joto la
bahari kuwa la juu ya wastani, mifumo ya upepo na mgandamizo wa hewa
vimeendelea kusababisha upungufu wa unyevunyevu katika anga.
Hali hii ya mabadiliko ya joto la bahari na mifumo ya hali ya hewa si ya kawaida na haijawahi kutokea katika miaka iliyopita.
Kutokana na
hali hii isiyokuwa ya kawaida taasisi zinazohusika na masuala ya hali
ya hewa katika Kanda ya Pembe ya Afrika (ICPAC) na Kanda ya Kusini mwa
Afrika (SADC-CSC) kwa mara ya kwanza zimeandaa warsha ya wataalamu wa
hali ya hewa ikiwemo Tanzania, kufanya uchambuzi wa mifumo ya hali ya
hewa na kutoa mrejeo wa mwelekeo wa mvua za msimu katika ukanda huu.
Mikutano
hii itafanyika tarehe 29 hadi 30 Novemba, 2012 Nairobi, Kenya na tarehe 5
hadi 13 Disemba, 2012 Lusaka, Zambia. Baada ya taarifa hiyo ya kikanda,
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itapitia taarifa hiyo na kutoa mrejeo
wa utabiri wa msimu wa mvua nchini.
Tathmini ya mvua kuanzia mwezi Oktoba hadi Novemba 2012:
Katika
maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka, hususani maeneo ya ukanda
wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na
Shinyanga) mvua zinaendelea kunyesha, wakati maeneo ya nyanda za juu
Kaskazini mashariki (mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) na pwani
ya Kaskazini (mikoa ya Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga na visiwa
vya Unguja na Pemba) kumekuwa na mvua ambazo ni za chini ya wastani.
Aidha,
katika maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka, hususani maeneo ya
Kigoma, Rukwa, Mbeya, Njombe, Iringa, Tabora, Katavi na Singida mvua
zimeanza na zinaendelea kunyesha. Mtawanyiko wa mvua hizo si wa
kuridhisha katika baadhi ya maeneo.
Ushauri:
Katika
maeneo ambayo mvua iliyonyesha mpaka sasa ni chini ya wastani, wananchi
wanashauriwa kutumia maji kwa uangalifu na kuhifadhi malisho kwa ajili
ya mifugo.
Pamoja na
mabadiliko hayo ambayo si ya kawaida yaliyojitokeza kuna uwezekano wa
kuwepo kwa vipingi vifupi vya mvua kubwa hivyo wananchi wanashauriwa
kuendelea kuchukua tahadhari.
Mamlaka ya hali ya hewa inaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na itaendelea kutoa taarifa “update” za mara kwa mara.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
No comments:
Post a Comment