Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Malawi Joyce Banda, wakitabasamu huku wakipeana mikono mara baada ya mazungumzo mjini Maputo
WAKATI Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
(UN), Ban K i – m o o n akipongeza msimamo wa Tanzania katika kutafuta
majawabu ya amani kuhusu mzozo wa mpaka kati yake na Malawi kwenye Ziwa
Nyasa, Rais Joyce Banda wa nchi hiyo ametangaza kwenda mahakamani.
Katika pongezi zake kwa Tanzania juzi,
Ban alisema uamuzi wa Tanzania ndiyo njia sahihi na inayokubaliwa
kimataifa kutafuta na kupata suluhisho la migogoro ya namna hiyo.
Lakini kwa upande wake, Rais Banda
alilitangazia Taifa lake kuwa analipeleka suala hilo katika Mahakama ya
Kimataifa (ICJ) ili haki iweze kutendeka, akiilaumu Tanzania kwa
alichodai ni kuchora ramani mpya ya Tanzania ikiwa na sehemu ya Ziwa
hilo.
Ban alitoa pongezi hizo kwa Tanzania
juzi alipokutana kwa mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko hapa,
kwa ziara ya siku mbili.
“Juzi nilikutana na Rais Banda wa Malawi
na akanielezea mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa
Nyasa na mazungumzo ambayo nchi zenu mbili zinafanya ili kupata ufumbuzi
wa amani.
Hii ndiyo njia sahihi na UN inaunga
mkono njia hiyo,” Ban alimweleza Rais Kikwete. Rais Kikwete naye
alimwambia Katibu Mkuu kuwa Tanzania bado inaamini kwamba njia sahihi ni
kutafuta ufumbuzi wa mvutano huo wa mpaka kwa njia ya mazungumzo.
Alisema: “Wazo la awali la kutafuta
ufumbuzi wa tatizo hili la miaka mingi sana lilitokana na Rais wa
Malawi, Bingu wa Mutharika ambaye ni marehemu, ambaye aliniandikia barua
ya kutaka nchi zetu zianze mazungumzo kuhusu mzozo huo.Nasi tulikubali.
Hivyo, ndivyo tulivyoanza kuzungumza.”
Rais Kikwete alisema Tanzania inaongozwa na msingi mkuu wa mipaka
inayopita kwenye maeneo ya maji ambako inakuwa katikati.
“Mpaka kati ya Malawi na Msumbiji kwenye
Ziwa hilo hilo, Nyasa, uko katikati ya Ziwa tangu mwaka 1954 wakati
nchi hizo zilipokubaliana kusahihisha makosa ya kuweka mpaka huo nje ya
Ziwa.
Mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye mto
mkubwa zaidi unaoingiza maji katika Ziwa Nyasa uko katikati ya mto
wenyewe,” alisema Rais Kikwete na kuongeza: “Kila mahali ambako nchi
zinatengenishwa na maji, mpaka unakuwa katikati ya nchi. Sisi tunadhani
hata kwenye mpaka wetu wa Malawi kwenye Ziwa Nyasa ni lazima uwe
katikati ya Ziwa.”
Alisema: “Katika hali ya sasa wananchi
wetu wanapokunywa maji ya Ziwa Nyasa wanakunywa maji ya Malawi, kila
watu wetu wanaposafiri ndani ya Ziwa kufanya shughuli zao wanasafiri
kwenye maji ya Malawi.Hili ni jambo linalohitaji majadiliano ya kuliweka
vizuri.”
Kauli ya Banda
Banda aliwaambia waandishi wa habari
juzi jijini Lilongwe, kwamba suala hili limefika mbali na Malawi sasa
itatafuta msaada wa kimataifa kuhakikisha kwamba haki inatendeka,
akisema Wamalawi hawawezi kuvumilia usumbufu kila wanapotaka kuvua ndani
ya Ziwa hilo.
“Suala hili la Ziwa limefikia hatua
nyingine. Nimeamua kulifikisha katika Mahakama ya Kimataifa ili kuamua
na kutatua mzozo huu,” Rais Banda alisema.
Banda alifafanua kuwa serikali kupitia
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, iliiandikia barua
Serikali ya Tanzania juu ya suala la kutoa ramani mpya ambayo inahusisha
sehemu ya Ziwa Nyasa.
Alisema mkutano mwingine ambao awali
ulikubalika ufanyike Tanzania, ulifutwa baada ya kubaini kwamba Tanzania
imetoa ramani mpya, akisema kama itajibu barua hiyo Malawi itaamua ama
kuendelea na mkutano huo au la.
“Tuliamua kufuta mkutano huo baada ya
kubaini kwamba Tanzania imetoa ramani mpya ikiwa na sehemu ya Ziwa letu.
Kama hawatajibu barua yetu tutatafuta njia nyingine,” alisema Rais huyo
aliyeingia madarakani mapema mwaka huu baada ya kifo cha Rais
Mutharika.
Ban asifu mchakato wa Katiba
Katika hatua nyingine, Ban alisifu na
kupongeza uamuzi wa Rais Kikwete wa kuandikwa upya kwa Katiba ya nchi.
Aidha, Ban alipongeza hatua ya amani na utulivu uliofikiwa Zanzibar
baada ya maridhiano na makubaliano ya kisiasa visiwani humo.
“Rais nakupongeza sana kwa uamuzi wako
sahihi na wa busara wa kisiasa wa kuangalia upya Katiba ya sasa ya nchi
yako kwa nia ya kutungwa Katiba mpya, kwa sababu hatua hiyo dhahiri
itaendeleza utulivu ambao umedumu Tanzania kwa miongo mingi,” Ban
alisema.
Ban alimwambia Rais Kikwete kuwa sasa
Tanzania na eneo lote la Afrika Mashariki linanufaika na uamuzi mwingine
wa busara wa kisiasa wa kutafuta na kupata maridhiano Zanzibar.
Alisifu jitihada zinazofanywa na
viongozi wa nchi wa eneo la Maziwa Makuu katika kuleta amani Mashariki
mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Niliitisha mkutano wa viongozi wa eneo
hilo Septemba 27, walihudhuria viongozi wengi akiwamo Rais Joseph Kabila
wa DRC na Rais Paul Kagame wa Rwanda, na kuwaeleza kuwa UN inafuatilia
kwa makini matukio ya eneo hilo na kuwajulisha kuwa kama wanahitaji
msaada wowote wa UN basi sisi tuko tayari,” alisema Ban.
Katibu Mkuu pia alimwomba Rais Kikwete
kusaidia maendeleo ya kisiasa Zimbabwe baada ya kuchaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Chombo Maalumu cha Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika (SADC) kuhusu Siasa, Ulinzi na Usalama.
“Kwa nafasi yako ya Mwenyekiti wa Chombo
Maalumu cha SADC ni dhahiri kuwa unaweza kuchangia sana naendeleo ya
kisiasa ya Zimbabwe,” alimwambia Rais Kikwete ambaye alikubaliana na
kauli ya Ban.
Rais alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa
uamuzi wa kuandika Katiba mpya unalenga kuwa na Katiba ambayo itaiongoza
Tanzania kwa miaka 50 ijayo.
“Baada ya kutumia Katiba yetu nzuri kwa
miaka 50 iliyopita, tukaamua kuwa pengine ni vema kuunda Katiba ambayo
itatupeleka kwa miaka mingine 50 ijayo. Naamini hili litatusaidia,”
alisema Rais Kikwete.
Chanzo. tabianchi.blogspot
Chanzo. tabianchi.blogspot
No comments:
Post a Comment