Serikali ya Tanzania, imeagiza mitihani yote ya kidato cha nne kwa mwaka
2012, kusahihishwa upya baada ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda ya kuchunguza sababu zilizosababisha matokeo ya kidato cha
nne mwaka 2012 kuwa mabaya, kuwahi kutokea katika historia ya mitihani
Tanzania.
Asilimia 60 ya watahiniwa walianguka mitihani hiyo na kusababisha
serikali kuunda tume ya uchunguzi baada ya wadau wa elimu, wazazi na
wanafunzi kulalamikia matokeo hayo.
Tume hiyo ilichunguza sababu zilizosabisha matokeo ya kidato cha nne
mwaka 2012 kuwa mabaya, na imependekeza kwa serikali kufuta matokeo yote
ya mitihani hiyo na isahihishwe upya.
Uamuzi huo umetangazwa katika kikao cha Bunge la Tanzania
linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu anaye shughulikia Sera na Uratibu, William Lukuvi.
Tume hiyo, ilipewa hadidu za rejea kadhaa ikiwemo kutafuta sababu za
matokeo mabaya ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012; Kubaini sababu
za kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika mitihani ya Kidato cha Nne
mwaka 2011 hadi 2012; Kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua kukabiliana
na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu mara
moja,kipindi cha muda mfupi, kati na kipindi cha muda mrefu.
Pia Tume hiyo ilipewa jukumu la kutathmini nafasi ya Halmashauri
katika kusimamia Elimu ya Sekondari katika Halmashauri zake; na kuanisha
sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali hii ya matokeo.
Tume imebaini pia kwamba, pamoja na Wanafunzi hawa kuwa katika
mazingira yanayofanana na ya wenzao wa miaka iliyopita na kwamba ufanisi
katika shule kwa ujumla umekuwa unashuka kwa sababu
mbalimbali,zikiwemo za mabadiliko ya mchakato wa kuandaa na kutoa
matokeo ya mtihani kwa mwaka 2012.
Mfumo uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia.
Hata hivyo baadhi ya wadau wa elimu, wazazi na wanafunzi wamehoji
uamuzi huo wa serikali kama hautakuwa na athari kwa wanafunzi waliofaulu
na kujiandaa na masomo ya kidato cha tano na wale ambao tayari
wamejiandikisha kurudia mitihani yao kwa njia ya kulipia
No comments:
Post a Comment